Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) limesema lina imani kuwa mazungumzo kati yake, Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
yatamaliza tatizo la kushikiliwa akaunti ya TFF kutokana na malipo ya kodi ya
mishahara ya makocha wa kigeni.
Rais wa TFF,
Leodegar Tenga alizungumza na waandishi wa habari jana juu
ya uamuzi wa TRA kushikilia akaunti ya TFF ikiielekeza Benki ya NMB kukata sh.
157,407,968 ikiwa ni malipo ya Kodi ya Mapato ya Mshahara wa Mfanyakazi (P.A.Y.E)
ya makocha Marcio Maximo na wasaidizi wake.
Katika mzozo huo wa
muda mrefu, TFF imejitetea kuwa haiwezi kulipa kodi hiyo kwa kuwa Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ndiyo mlipaji wa mishahara ya makocha
hao, ikiwa ni ahadi ya Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete ya kulipia makocha wa
michezo tofauti, ukiwemo mpira wa miguu.
“Hili ni suala nyeti
ambalo linahitaji kumalizwa kwa mazungumzo baina ya pande zote. Ninataka
kuwahakikishia kuwa suala hili linazungumzwa na tayari nimeshafanya
mazungumzo na maofisa wa Wizara na tumekubaliana kukutana na pande zote
wakati wowote; iwe leo jioni au kesho.
“Ni matumaini yangu
kuwa suala hili litakwisha na nimetoka Kampala (Uganda kwenye Kombe la
Chalenji) moja kwa moja na kwenda kuzungumza na viongozi wa Wizara na
wamekubali kwamba tuongee pande zote kulimaliza suala hili.
“Nimezungumza na
wenzetu wa Serikali kwa sababu najua unyeti wa suala hili. Fedha zilizokamatwa
si zetu; ni fedha za klabu na zimetolewa na mdhamini ambaye tumekubaliana
namna ya kuzitumia. Fedha hizi hazikutolewa kwa ajili ya kulipia kodi. Lakini
TRA wanazishikilia kwa sababu Premier League iko chini ya TFF,” amesema Rais
Tenga.
Tenga amesema TRA
wanafanya kazi kwa kufuata sheria zao za ukataji kodi na hivyo wana haki ya
kufuatilia kwa kuwa kwa mujibu wa sheria, mwajiri ndiye anayetakiwa kukata
kodi kutoka kwenye mshahara wa mfanyakazi.
|
No comments:
Post a Comment